UTUNZAJI WA MAZINGIRA
1.0 UTANGULIZI
Kutokana na changamoto kubwa tuliyo nayo ya mabadiliko ya tabia nch, leo nimeshawishika niandike kwa kifupi kile ambacho Mungu anataka tukijue kuhusu mazingira.
“BWANA Mungu akamtwaa huyo
mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” (Mwanzo 2: 15)
Wapendwa, nitumie
nafasi hii kuwakumbusha kuwa, Mungu anatukumbusha juu ya nchi nzuri aliyokuwa ameifanya na
kumkabidhi mwanadamu ili aitunze. Neno hili linatujia wakati ambao tunakabiliwa
na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira. Ardhi tuliyozoea zamani ikitoa
mazao yakutosha na bora kwa chakula na biashara sasa imechoka, mabadiliko
makubwa ya hali ya hewa, mazingira yetu yaliyokuwa na ubaridi uliovutia, sasa
yana joto linalozidi miji yote katika bara letu la Afrika. Mlima Kilimanjaro
tuliozoea kuuona umefunikwa na theluji na kuvutia macho ya kila aliyeutazama
sasa unaelekea kuonekana kama mchanga
uliokusanywa unaosubiri mnunuzi, miti iliyopamba mazingira yetu kwa rangi nzuri
ya kijani na kutupa kivuli kizuri sasa inaelekea kuisha. Tunakabiliwa na hatari
kubwa ya kutoweka kwa miti na mimea ya asili iliyotambulisha maeneo yetu
ulimwenguni. Kila mahali walitambua kuwa mruka, msesewe n.k ni miti ya
Kilimanjaro. Maparachichi yalipatakana kwa wingi Kilimanjaro kuliko mahali
pengine katika nchi yetu. Kahawa aina ya Arabica iliyostawi kwa wingi katika mkoa
wetu kuliko mikoa mingine, na yenyewe ipo hatarini kutoweka. Haya yote ni
madhara yatokanayo na uharibifu mkubwa wa mazingira. Swali la kujiuliza ni
hili; “Je! tunayaona haya yanayoendelea katika mazingira yetu, au tumefunga
macho yetu ili tusione uhalisia wa tunakoelekea?” Ndugu zangu, inabidi
tufunguke macho tuone na kuchukua hatua ya kuurejesha uumbaji wa Mungu katika
uhalisia wake. Huu ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuanzia mtoto mdogo mpaka
mzee.
Mwanaharakati maarufu wa mazingira, Hayati Prof. Wangari Mathai
akihamasisha utunzaji wa mazingira na hasa misitu alisema; “Misitu imechangia sana katika ukombozi wa mwanadamu, kwani,
hata msalaba wa Yesu, yupo mtu aliyekwenda msituni akakata mti wa
kuutengenezea.”
Wapendwa, alichotaka ndugu yetu huyu tufahamu ni umuhimu wa
kutunza mazingira, kwani, “mazingira ni
uhai.” Ukataji miti umefanywa hata kwenye vyanzo vya maji na hivyo
kusababisha uhaba mkubwa wa maji katika mazingira yetu. Wakati mwingine twaweza
kutiwa moyo na maji kidogo yaliyopo na kufikiri hali ni nzuri, lakini hebu
jiulize, twaweza kupata tena maji hata ya kumwagilia bustani ndogo tu ya mboga?
Hata yakipatikana ni kwa wachache na siyo wengi kama
ilivyokuwa mwanzo.
Wapendwa, kinachohitajika
sasa, ni kila mmoja wetu kukubali kufumbuliwa macho ya mioyo yetu kuiona hatari
ya kimazingira inayotukabili. Tukiruhusu hali hii iliyopo kuendelea tutajikuta
wakati mmoja kama siyo sisi vizazi vijavyo,
tukiishi jangwani mahali pasipokuwa na maji wala uhakika wa chakula. Katika
hili hatuhitaji msaada kutoka kwa wafadhili bali jitahada zetu wenyewe kwa
msaada wa Mungu, zitazaa matunda. Naomba nikuachie changamoto hii; “Umepanda miti mingapi na umezuia miti
mingapi kukatwa?”
Mwisho, sote tujitoe kuwa
walinzi wa mazingira na kumuona kila asiyependa kutunza mazingira, kuwa mtu
hatari, adui mkubwa na muuaji, kwani, madhara anayoyasababisha ni makubwa
yaani, vifo kwa wanadamu, wanyama na mimea.
Nikushawishi Mpendwa msomaji wangu, uwe miongoni mwa wanaharakati wa mazingira po pote ulipo, si kwa wale wa Kilimanjaro tu.
Mungu akubariki sana.
1 comment:
Mazingira ni muhimu sana
Post a Comment