Friday, 22 July 2016

UTUNZAJI WA MAZINGIRA

1.0 UTANGULIZI




Kutokana na changamoto kubwa tuliyo nayo ya mabadiliko ya tabia nch, leo nimeshawishika niandike kwa kifupi kile ambacho Mungu anataka tukijue kuhusu mazingira.

“BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” (Mwanzo 2: 15)

Wapendwa, nitumie nafasi hii kuwakumbusha kuwa, Mungu anatukumbusha juu ya nchi nzuri aliyokuwa ameifanya na kumkabidhi mwanadamu ili aitunze. Neno hili linatujia wakati ambao tunakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira. Ardhi tuliyozoea zamani ikitoa mazao yakutosha na bora kwa chakula na biashara sasa imechoka, mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, mazingira yetu yaliyokuwa na ubaridi uliovutia, sasa yana joto linalozidi miji yote katika bara letu la Afrika. Mlima Kilimanjaro tuliozoea kuuona umefunikwa na theluji na kuvutia macho ya kila aliyeutazama sasa unaelekea kuonekana kama mchanga uliokusanywa unaosubiri mnunuzi, miti iliyopamba mazingira yetu kwa rangi nzuri ya kijani na kutupa kivuli kizuri sasa inaelekea kuisha. Tunakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka kwa miti na mimea ya asili iliyotambulisha maeneo yetu ulimwenguni. Kila mahali walitambua kuwa mruka, msesewe n.k ni miti ya Kilimanjaro. Maparachichi yalipatakana kwa wingi Kilimanjaro kuliko mahali pengine katika nchi yetu. Kahawa aina ya Arabica iliyostawi kwa wingi katika mkoa wetu kuliko mikoa mingine, na yenyewe ipo hatarini kutoweka. Haya yote ni madhara yatokanayo na uharibifu mkubwa wa mazingira. Swali la kujiuliza ni hili; “Je! tunayaona haya yanayoendelea katika mazingira yetu, au tumefunga macho yetu ili tusione uhalisia wa tunakoelekea?” Ndugu zangu, inabidi tufunguke macho tuone na kuchukua hatua ya kuurejesha uumbaji wa Mungu katika uhalisia wake. Huu ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuanzia mtoto mdogo mpaka mzee.

Mwanaharakati maarufu wa mazingira, Hayati Prof. Wangari Mathai akihamasisha utunzaji wa mazingira na hasa misitu alisema; “Misitu imechangia sana katika ukombozi wa mwanadamu, kwani, hata msalaba wa Yesu, yupo mtu aliyekwenda msituni akakata mti wa kuutengenezea.” 

Wapendwa, alichotaka ndugu yetu huyu tufahamu ni umuhimu wa kutunza mazingira, kwani, “mazingira ni uhai.” Ukataji miti umefanywa hata kwenye vyanzo vya maji na hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa maji katika mazingira yetu. Wakati mwingine twaweza kutiwa moyo na maji kidogo yaliyopo na kufikiri hali ni nzuri, lakini hebu jiulize, twaweza kupata tena maji hata ya kumwagilia bustani ndogo tu ya mboga? Hata yakipatikana ni kwa wachache na siyo wengi kama ilivyokuwa mwanzo.

Wapendwa, kinachohitajika sasa, ni kila mmoja wetu kukubali kufumbuliwa macho ya mioyo yetu kuiona hatari ya kimazingira inayotukabili. Tukiruhusu hali hii iliyopo kuendelea tutajikuta wakati mmoja kama siyo sisi vizazi vijavyo, tukiishi jangwani mahali pasipokuwa na maji wala uhakika wa chakula. Katika hili hatuhitaji msaada kutoka kwa wafadhili bali jitahada zetu wenyewe kwa msaada wa Mungu, zitazaa matunda. Naomba nikuachie changamoto hii; “Umepanda miti mingapi na umezuia miti mingapi kukatwa?”

Mwisho, sote tujitoe kuwa walinzi wa mazingira na kumuona kila asiyependa kutunza mazingira, kuwa mtu hatari, adui mkubwa na muuaji, kwani, madhara anayoyasababisha ni makubwa yaani, vifo kwa wanadamu, wanyama na mimea.

Nikushawishi Mpendwa msomaji wangu, uwe miongoni mwa wanaharakati wa mazingira po pote ulipo, si kwa wale wa Kilimanjaro tu. 

Mungu akubariki sana.

1 comment:

Unknown said...

Mazingira ni muhimu sana