MWISHO WA SAFARI YA MAISHA YA MCH. ALBERT G. MBOYA
TAREHE 26 AGOSTI, 2015
TAREHE 26 AGOSTI, 2015
Mch. Albert G. Mboya alikuwa miongoni mwa Wachungaji wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, aliyetumika katika Usharika wa Mang'ola uliopo Jimbo la Karatu.
Mch. Albert G. Mboya alizaliwa katika eneo la Olmolog Wilayani Siha tarehe 10 Mei, 1974 akiwa ni mtoto wa Bw. & Bibi Gadieli Mboya ambao ni wakazi wa Olmolog wenye asili ya Nkweshoo Machame.
Alikuwa miongoni mwa Wachungaji vijana kwani, hakuwa na muda mrefu katika huduma ya Uchungaji kwani alibarikiwa kuwa Mchungaji tarehe 23 Novemba, 2014 katika Ibada iliyofanyika Usharika wa Oshara Jimbo la Siha na pia bado kiumri alikuwa na umri wa miaka 41.
Kabla ya kusoma masomo ya Theologia na kubarikiwa kuwa Mchungaji, Marehemu Mch. Albert Mboya alitumika kwa kipindi kifupi kama Mwinjilisti katika Usharika wa Olmolog baada ya kuhitimu masomo yake ya Kozi ya Kawaida ya Uinjilisti katika Chuo cha Biblia Mwika.
Mchungaji alianza kupata maumivu ya tumbo ndani ya kipindi cha majuma mawili, na kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Masista Magadini Siha na Hospitali Teule Kilutheri iliyopo Wilaya ya Karatu, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC baada ya hali yake ya afya kuzidi kuwa mbaya.
Wakati akiendelea na matibabu iligundulika kuwa amepatwa na tatizo ambalo kitaalamu linajulikana kama "Hypovolemic Shock" lililosababishwa na kupasuka kwa mshipa wa damu katika koromeo na kusababisha damu kuvujia tumboni, tatizo lililopelekea Mchungaji kutapika na kuharisha damu na hatimaye kuwa na tatizo la kuishiwa damu "Anaemia" na hatimaye kusababisha umauti wake siku ya Jumatano majira ya saa 12 asubuhi ya tarehe 26 Agosti, 2015 katika hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Marehemu Mch. Albert Mboya alizikwa siku ya Jumamosi tarehe 29 Agosti, 2015 katika Usharika wa Wiri Mtaa wa Mlangoni katika Ibada iliyoongozwa na Baba Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Martin F. Shao akishirikiana na Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Elingaya A. Saria, Baba Askofu Dkt. Gideon Maghina wa Redio Sauti ya Injili, Wakuu wa Majimbo ya Siha (Mch. Elisa A. Kileo), Hai (Mch. Aminarabi Swai), Karatu (Mch. Samweli Slaa), Kilimanjaro Kati (Mch. Kennedy Kisanga) pamoja na Wachungaji toka sharika na vituo mbalimbali vya Dayosisi. Wengine waliohudhuria Ibada hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Bw. Julius Mosi, Mama Askofu (Janeth F. Shoo), Mama Msaidizi wa Askofu (Yohana E. Saria) na Naibu Waziri wa TAMISEMI Bw. Aggrey D. Mwanri. Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na mamia ya Wakristo na waumini wa dini mbalimbali, waliohudumiwa kijamii na kiroho na Marehemu Mch. Albert Mboya.
Marehemu Mch. Albert Mboya ameacha mke mjane aitwaye Anna Mwafifi na watoto wawili ambao ni Glory na Danieli.
WASIFU
Kwa watu wa Karibu na Marehemu Mch. Mboya, wanamkumbuka kwa upole na utulivu wake. Mtu aliyependa kutafuta ushauri na kuelekezwa kwa lile aliloona hafahamu. Mchungaji aliyekuwa na mzigo wa kuwahudumia Wakristo na wasio Wakristo kiakili, kiroho na kijamii.
Alikuwa Mchungaji kweli kweli, aliyeipenda huduma yake na hasa katika kufundisha na kuhubiri kwa usahihi Neno la Mungu kwa marika yote.
Ni Mchungaji aliyeshirikiana vizuri na watu wote bila kujali mikazo ya kimadhehebu. Hili lilishuhudiwa na umati wa watu wa madhehebu na dini mbalimbali waliohudhuria mazishi yake, wakitokea maeneo aliyowahi kuishi kama vile West Kilimanjaro na Mang'ola alikotoa huduma kama Mchungaji na pia Msaranga Mandaka alikofanyia mazoezi ya huduma ya Kichungaji.
Katika yote tunachoweza kusema ni "BWANA ametoa na BWANA ametwaa, jina la BWANA lihimidiwe.
PICHA MBALIMBALI ZA TUKIO LA MAZISHI YA MCH. ALBERT MBOYA
Pichani ni baadhi ya Wachungaji wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini na waombolezaji wengine waliohudhuria Ibada ya mazishi ya Marehemu Mch. Albert Mboya
Baba Askofu Dkt. Gideon Maghina wa Radio Sauti ya Injili akihubiri katika Ibada ya mazishi ya Mch. Albert G. Mboya
Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Bw. Julius Mosi akitambulisha wageni na makundi mbalimbali ya waombolezaji.
Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Elingaya A. Saria akiwakaribisha baadhi ya Viongozi wa Kanisa na Serikali kutoa salamu za rambirambi
Baba Askofu Mstaafu Dkt. Martin F. Shao, Naibu Waziri TAMISEMI (Bw. Aggrey Mwanri) pamoja na familia, wakiuaga mwili wa Marehemu Mch. Albert G. Mboya
Baba Askofu Mstaafu Dkt. Martin F. Shao, akiongoza Liturgia ya makaburini katika mazishi ya Marehemu Mch. Albert G. Mboya
Vijana wakiliteremsha katika kaburi jeneza lenye mwili wa Marehemu Mch. Albert G. Mboya
Wachungaji wakipamba maua kwenye kaburi la Marehemu Mch. Albert G. Mboya
No comments:
Post a Comment