Friday, 22 July 2016

UTUNZAJI WA MAZINGIRA

1.0 UTANGULIZI




Kutokana na changamoto kubwa tuliyo nayo ya mabadiliko ya tabia nch, leo nimeshawishika niandike kwa kifupi kile ambacho Mungu anataka tukijue kuhusu mazingira.

“BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” (Mwanzo 2: 15)

Wapendwa, nitumie nafasi hii kuwakumbusha kuwa, Mungu anatukumbusha juu ya nchi nzuri aliyokuwa ameifanya na kumkabidhi mwanadamu ili aitunze. Neno hili linatujia wakati ambao tunakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira. Ardhi tuliyozoea zamani ikitoa mazao yakutosha na bora kwa chakula na biashara sasa imechoka, mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, mazingira yetu yaliyokuwa na ubaridi uliovutia, sasa yana joto linalozidi miji yote katika bara letu la Afrika. Mlima Kilimanjaro tuliozoea kuuona umefunikwa na theluji na kuvutia macho ya kila aliyeutazama sasa unaelekea kuonekana kama mchanga uliokusanywa unaosubiri mnunuzi, miti iliyopamba mazingira yetu kwa rangi nzuri ya kijani na kutupa kivuli kizuri sasa inaelekea kuisha. Tunakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka kwa miti na mimea ya asili iliyotambulisha maeneo yetu ulimwenguni. Kila mahali walitambua kuwa mruka, msesewe n.k ni miti ya Kilimanjaro. Maparachichi yalipatakana kwa wingi Kilimanjaro kuliko mahali pengine katika nchi yetu. Kahawa aina ya Arabica iliyostawi kwa wingi katika mkoa wetu kuliko mikoa mingine, na yenyewe ipo hatarini kutoweka. Haya yote ni madhara yatokanayo na uharibifu mkubwa wa mazingira. Swali la kujiuliza ni hili; “Je! tunayaona haya yanayoendelea katika mazingira yetu, au tumefunga macho yetu ili tusione uhalisia wa tunakoelekea?” Ndugu zangu, inabidi tufunguke macho tuone na kuchukua hatua ya kuurejesha uumbaji wa Mungu katika uhalisia wake. Huu ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuanzia mtoto mdogo mpaka mzee.

Mwanaharakati maarufu wa mazingira, Hayati Prof. Wangari Mathai akihamasisha utunzaji wa mazingira na hasa misitu alisema; “Misitu imechangia sana katika ukombozi wa mwanadamu, kwani, hata msalaba wa Yesu, yupo mtu aliyekwenda msituni akakata mti wa kuutengenezea.” 

Wapendwa, alichotaka ndugu yetu huyu tufahamu ni umuhimu wa kutunza mazingira, kwani, “mazingira ni uhai.” Ukataji miti umefanywa hata kwenye vyanzo vya maji na hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa maji katika mazingira yetu. Wakati mwingine twaweza kutiwa moyo na maji kidogo yaliyopo na kufikiri hali ni nzuri, lakini hebu jiulize, twaweza kupata tena maji hata ya kumwagilia bustani ndogo tu ya mboga? Hata yakipatikana ni kwa wachache na siyo wengi kama ilivyokuwa mwanzo.

Wapendwa, kinachohitajika sasa, ni kila mmoja wetu kukubali kufumbuliwa macho ya mioyo yetu kuiona hatari ya kimazingira inayotukabili. Tukiruhusu hali hii iliyopo kuendelea tutajikuta wakati mmoja kama siyo sisi vizazi vijavyo, tukiishi jangwani mahali pasipokuwa na maji wala uhakika wa chakula. Katika hili hatuhitaji msaada kutoka kwa wafadhili bali jitahada zetu wenyewe kwa msaada wa Mungu, zitazaa matunda. Naomba nikuachie changamoto hii; “Umepanda miti mingapi na umezuia miti mingapi kukatwa?”

Mwisho, sote tujitoe kuwa walinzi wa mazingira na kumuona kila asiyependa kutunza mazingira, kuwa mtu hatari, adui mkubwa na muuaji, kwani, madhara anayoyasababisha ni makubwa yaani, vifo kwa wanadamu, wanyama na mimea.

Nikushawishi Mpendwa msomaji wangu, uwe miongoni mwa wanaharakati wa mazingira po pote ulipo, si kwa wale wa Kilimanjaro tu. 

Mungu akubariki sana.

Wednesday, 2 September 2015

MWISHO WA SAFARI YA MAISHA YA MCH. ALBERT G. MBOYA 
TAREHE 26 AGOSTI, 2015
Mch. Albert G. Mboya alikuwa miongoni mwa Wachungaji wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, aliyetumika katika Usharika wa Mang'ola uliopo Jimbo la Karatu.
Mch. Albert G. Mboya alizaliwa katika eneo la Olmolog Wilayani Siha tarehe 10 Mei, 1974 akiwa ni mtoto wa Bw. & Bibi Gadieli Mboya ambao ni wakazi wa Olmolog wenye asili ya Nkweshoo Machame.
Alikuwa miongoni mwa Wachungaji vijana kwani, hakuwa na muda mrefu katika huduma ya Uchungaji kwani alibarikiwa kuwa  Mchungaji tarehe 23 Novemba, 2014 katika Ibada iliyofanyika Usharika wa Oshara Jimbo la Siha na pia bado kiumri alikuwa na umri wa miaka 41.
Kabla ya kusoma masomo ya Theologia na kubarikiwa kuwa Mchungaji, Marehemu Mch. Albert Mboya alitumika kwa kipindi kifupi kama Mwinjilisti katika Usharika wa Olmolog baada ya kuhitimu masomo yake ya Kozi ya Kawaida ya Uinjilisti katika Chuo cha Biblia Mwika.
Mchungaji alianza kupata maumivu ya tumbo ndani ya kipindi cha majuma mawili, na kupatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Masista Magadini Siha na Hospitali Teule Kilutheri iliyopo Wilaya ya Karatu, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC baada ya hali yake ya afya kuzidi kuwa mbaya.
Wakati akiendelea na matibabu iligundulika kuwa amepatwa na tatizo ambalo kitaalamu linajulikana kama "Hypovolemic Shock" lililosababishwa na kupasuka kwa mshipa wa damu katika koromeo na kusababisha damu kuvujia tumboni, tatizo lililopelekea Mchungaji kutapika na kuharisha damu na hatimaye kuwa na tatizo la kuishiwa damu "Anaemia" na hatimaye kusababisha umauti wake siku ya Jumatano majira ya saa 12 asubuhi ya tarehe 26 Agosti, 2015 katika hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Marehemu Mch. Albert Mboya alizikwa siku ya Jumamosi tarehe 29 Agosti, 2015 katika Usharika wa Wiri Mtaa wa Mlangoni katika Ibada iliyoongozwa na Baba Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Martin F. Shao akishirikiana na Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Elingaya A. Saria, Baba Askofu Dkt. Gideon Maghina wa Redio Sauti ya Injili, Wakuu wa Majimbo ya Siha (Mch. Elisa A. Kileo), Hai (Mch. Aminarabi Swai), Karatu (Mch. Samweli Slaa), Kilimanjaro Kati (Mch. Kennedy Kisanga) pamoja na Wachungaji toka sharika na vituo mbalimbali vya Dayosisi. Wengine waliohudhuria Ibada hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Bw. Julius Mosi, Mama Askofu (Janeth F. Shoo), Mama Msaidizi wa Askofu (Yohana E. Saria) na Naibu Waziri wa TAMISEMI Bw. Aggrey D. Mwanri. Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na mamia ya Wakristo na waumini wa dini mbalimbali, waliohudumiwa kijamii na kiroho na Marehemu Mch. Albert Mboya.
Marehemu Mch. Albert Mboya ameacha mke mjane aitwaye Anna Mwafifi na watoto wawili ambao ni Glory na Danieli.
WASIFU
Kwa watu wa Karibu na Marehemu Mch. Mboya, wanamkumbuka kwa upole na utulivu wake. Mtu aliyependa kutafuta ushauri na kuelekezwa kwa lile aliloona hafahamu. Mchungaji aliyekuwa na mzigo wa kuwahudumia Wakristo na wasio Wakristo kiakili, kiroho na kijamii.
Alikuwa Mchungaji kweli kweli, aliyeipenda huduma yake na hasa katika kufundisha na kuhubiri kwa usahihi Neno la Mungu kwa marika yote.
Ni Mchungaji aliyeshirikiana vizuri na watu wote bila kujali mikazo ya kimadhehebu. Hili lilishuhudiwa na umati wa watu wa madhehebu na dini mbalimbali waliohudhuria mazishi yake, wakitokea maeneo aliyowahi kuishi kama vile West Kilimanjaro na Mang'ola alikotoa huduma kama Mchungaji na pia Msaranga Mandaka alikofanyia mazoezi ya huduma ya Kichungaji.
Katika yote tunachoweza kusema ni "BWANA ametoa na BWANA ametwaa, jina la BWANA lihimidiwe.
PICHA MBALIMBALI ZA TUKIO LA MAZISHI YA MCH. ALBERT MBOYA
Pichani ni baadhi ya Wachungaji wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini na waombolezaji wengine waliohudhuria Ibada ya mazishi ya Marehemu Mch. Albert Mboya

Baba Askofu Dkt. Gideon Maghina wa Radio Sauti ya Injili akihubiri katika Ibada ya mazishi ya Mch. Albert G. Mboya

Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Bw. Julius Mosi akitambulisha wageni na makundi mbalimbali ya waombolezaji.


Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Elingaya A. Saria akiwakaribisha baadhi ya Viongozi wa Kanisa na Serikali kutoa salamu za rambirambi




Baba Askofu Mstaafu Dkt. Martin F. Shao, Naibu Waziri TAMISEMI (Bw. Aggrey Mwanri) pamoja na familia, wakiuaga mwili wa Marehemu Mch. Albert G. Mboya



Baba Askofu Mstaafu Dkt. Martin F. Shao, akiongoza Liturgia ya makaburini katika mazishi ya Marehemu Mch. Albert G. Mboya




Vijana wakiliteremsha katika kaburi jeneza lenye mwili wa Marehemu Mch. Albert G. Mboya

Wachungaji wakipamba maua kwenye kaburi la Marehemu Mch. Albert G. Mboya













Thursday, 27 August 2015

Wapendwa ndugu zangu,
My Beloved,

Ninamshukuru Mungu ambaye ametujalia uzima na kutupa vipawa mbalimbali. Ninapenda kuwajulisha rasmi kuwa hii ni blog yangu.
I thank God who awards us life and different gifts. I would like officially to inform you about my blog.

Kupitia blog hii nitawajulisha matukio mbalimbali ya kikanisa na pia mafundisho ya Neno la Mungu.
Through this blog I will share with you different church events and teaching the Word of God.

Ninawakaribisha sana,
Your warmly welcome

Mungu awabariki.
May God bless you.